Friday, 29 July 2016

HABARI LEO



DAR ES SALAAM
OPERESHENI Ukuta iliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itakayokwenda sambamba na mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi, imezua taharuki miongoni mwa makundi mbalimbali nchini.
Akitangaza uamuzi huo juzi Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema operesheni hiyo ina lengo la kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia aliyoda kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli dhidi ya makundi mengine ya kisiasa na kijamii.
Mbowe alisema Kamati Kuu ya chama hicho imeainisha hoja 24 za chimbuko la Ukuta (Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania), mojawapo ikiwa ni hatua ya Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano yote ya hadhara ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.
Siku moja baada ya tamko hilo, Msajili wa vyama vya siasa nchini, jaji Francis Mutungi ametoa taarifa ya kulaani tamko hilo la Chadema akisema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, kuudhi na linahamasisha vurugu na uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Chadema kuzingatia sheria kwa kutii zuio la mikutano ya hadhara lililotolewa na Jeshi la Polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, amesema Chadema wanapotosha umma kwani Serikali haijazuia mikutano ya kikatiba kwenye majimbo yao.
Wakati Sendeka akisema hivyo, wabunge wa Chadema, Wilbroad Qambalo (Karatu) na Cesilia Pareso (Viti Maalumu), walihojiwa juzi na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kosa la kufanya mikutano na wananchi bila kibali cha polisi.
Mbali na Chadema, taarifa ya ziara zinazotarajiwa kufanywa na Rais Magufuli, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, Singida na Kahama mkoani Shinyanga kwa lengo la kuwashukuru wananchi kumpigia kura Oktoba mwaka jana, imepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wasomi, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa na baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza wamesema kitendo cha rais kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano wakati yeye akifanya mikutano kimetokana na udhaifu wa katiba ya mwaka 1977 inayotumika sasa.

GEITA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza katika Mgodi wa Dhahabu wa Nyamahuna mkoani  Geita na kukuta Wachina 72 kati ya 100 wakiishi na kufanya kazi bila vibali.
Akizungumza katika mgodi huo unaomilikiwa na Mtanzania, Andrew Obole, Mwigulu amesema alifika hapo kutokana na kuona taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya jamii zikimuonyesha Masanja Shokera akicharazwa bakora na raia wa mmoja wa China, Lee Swii, kwa madai ya kuiba mawe ya dhahabu Julai 6, mwaka huu.
Amesema taarifa alizonazo ambazo zipo uhamiaji zinaonyesha kuwa raia wa China waliopo mgodini hapo ni 28 ambao wana vibali halali vya kuishi nchini.
Waziri amesema kwa sababu hiyo, ameagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita kuwaweka chini ya ulinzi Wachina wengine 72, walinzi saba na Kaimu Meneja Uzalishaji, Richard Joachim.
Vilevile  huyo anayeitwa Lee ambaye anatuhumiwa kumdhalilisha Mtanzania ameamriwa awekwe chini ya ulinzi na walinzi saba.
Masanja Shokera anayedaiwa kudhalilishwa,  , amesema  siku hiyo alivamiwa na walinzi wa mgodi huo  akituhumiwa kuiba mawe ya dhahabu.
Amesema walimpiga  na kumfunga mikono na miguu na kuendelea kumwadhibu hali iliyosababisha apoteze fahamu.
Mkurugenzi wa mgodi huo, Andrew Obole amesema anachotambua Wachina waliopo kwake ni 28 na kwamba hao wengine alikuwa hawatambui.
DAR ES SALAAM
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezindua Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara kwa Mwaka 2015 ambacho kimebainisha kuwa asilimia 60 ya wafanyakazi nchini hawana Mikataba stahiki ya kazi, jambo linalosababisha serikali kupoteza mapato ya kodi.
Aidha ripoti imebainisha Mikataba mingine iliyopo kuwa na upungufu mwingi ikiwa ni pamoja na miongoni mwao kuandikwa kwa lugha isiyoeleweka na mingine kuandikwa kwa ufupi na kushindwa kujumuisha mambo ya msingi.
Nalo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), limekiri kuwepo kwa matatizo hayo kwa wafanyakazi lakini likafafanua kuwa wengi ni waoga kufukuzwa kazi, hivyo wanashindwa kujitokeza hadharani na kueleza yanayowasibu.
Akizungumzia ripoti hiyo wakati wa uzinduzi jijini Dar es Salaam jana, Mtafiti wa Taarifa wa LHRC Clarence Kipobota amesema miongoni mwa wafanyakazi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kukosa Mikataba halali ya kazi ni pamoja na waandishi wa habari pamoja na madereva.
Amesema kutokuwepo pia kwa vyama vya wafanyakazi katika maeneo ya kazi, kumekuwa kukichangia wengi wao kukosa makubaliano ya pamoja.
DODOMA
RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Dk James Wanyancha.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi iliyotolewa mjini Dodoma jana imesema Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kuanzia Julai 28, 2016.
Imesema kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Joseph Odo Haule kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Balozi Kijazi, uteuzi wa Haule umeanza jana Julai 28.
Kabla ya uteuzi huo Haule alikuwa Meneja wa Mfuko wa Barabara. Wajumbe wengine wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wanaendelea katika nafasi zao.

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis (79) jana alianguka wakati wa ibada,   kwenye madhabahu ya Jasna Gora, mjini Czestoshowa, Poland.
Tukio hilo lilitokea  baada ya Papa Francis kujiikwaa akiwa madhabahuni hali iliyowalazimu mapadre waliokuwa karibu naye kumsaidia kuinuka.
Taarifa zinasema Papa alianguka chini karibu na ngazi za madhabahuni na aliinuliwa na mapadri waliokuwa kwenye misa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za utabibu, Papa Francis amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa sciatica unaosababishwa na  maumivu chini ya mgongo.
Papa Francis, ambaye ni mzaliwa wa  Argentina alionekana akitembea huku akitafakari  hali iliyomfanya asigundue kuwa kulikuwa na ngazi mbele yake.
Baad ya kuinuka, Papa Francis, aliendelea na taratibu za ibada kama ilivyopangwa.
Alihubiri kwa muda mrefu kwenye ibada hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini huku ikifuatiliwa pia na mamilioni ya waumini wa dhehebu hilo, kwa njia ya runinga.
Msemaji wa Vatican, Greg Burke, aliwaambia waandishi wa habari   kuwa kiongozi huyo yuko salama na hakuna maumivu yoyote aliyoyapata alipoanguka.
Papa Francis aliwahi kuteleza na hata kuanguka mara kadhaa   na kila mara huwa anainuka peke yake au kusaidiwa na mmoja wa wasaidizi wake,
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani aliendesha   ibada katika kituo cha utawa ambayo ni nyumba maarufu ya watu kale  kwa Kanisa   Katoliki.
Katika ibada hiyo, ulinzi ulikuwa mkali kutokana muendelezo wa mashambulio ya ugaidi barani Ulaya.
Wanajeshi na polisi walionekana maeneo mbalimbali ya barabara katika ziara hiyo ya siku tano nchini Poland.

Hillary Clinton amekubali rasmi kuwa mgombezi wa Urais wa Marekani kupitia chama cha Democratic, huku akisema wakati wa kupambana na mpinzani wake sasa umeanza rasmi.
Alitoa wito kwa wanachama wote wa Democratic kuungana naye huku akimkebehi mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump, katika madai yake kuwa ni yeye pekee anayeweza kuyasuluhisha matatizo ya Marekani.
Alisema kuwa Wamarekani hufanya kazi kwa pamoja kyatatua yote yanayonufaisha taifa.
Awali, bintiye Chelsea Clinton alikuwa ametoa hotuba na kumsifu sana mamake. Alisema ni mwanamke ambaye huwa hasahau anawapigania akina nani.
"Watu huniuliza kila wakati, huwa anawezaje kufanya haya? ... ni kwa sababu huwa hawasahau watu anaowatetea," amesema.
"Najua kwa moyo wangu wote kwamba mamangu atatufanya tujionee fahari."

Mke wa mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donal Trump, Melania, amefuta tovuti yake baada ya vyombo vya habari nchini Marekani kuanza kutilia shaka ukweli wa baadhi ya madai yake.
Bi Trump amesema tovuti hiyo imefutwa kwa sababu haikuwa inaashiria wala kuonyesha mambo anayoangazia kwa sasa.
Vyombo vya habari nchini Marekani vilikuwa vimetilia shaka ukweli wa madai kwamba ana shahada katika usanifu mijengo kutoka chuo kikuu kimoja nchini Slovenia, kama alivyokuwa ameandika katika wasifu wake mtandaoni.
Kitabu kuhusu maisha yake kilichochapishwa mwaka huu kinasema aliacha masomo baada ya mwaka mmoja kuangazia kazi ya uanamitindo.
Wiki iliyopita, Melania Trump, alishutumiwa vikali baada ya hotuba aliyoitoa kwenye Kongamano kuu la chama cha Republican, kudaiwa kuwa kukopa sana maneno kutoka kwa hotuba iliyotolewa na mke wa rais wa sasa Michelle Obama katika kongamano la chama cha Democratic miaka minane iliyopita

No comments: